Wednesday, 19 July 2017

Ijue Shule ya Sekondari Njinjo

1. MAHALI ILIPO
Shule ya sekondari Njinjo ni shule ya serikali iliyopo mkoa wa Lindi wilaya ya Kilwa, kata ya Njinjo Kijijini Kipindimbi. Ni pwani ya Tanzania na ipo km 96 kutoka makao makuu ya wilaya ya Kilwa-Kilwa masoko. Shule ipo inapatikana ndani ya tarafa ya Njinjo yenye kata tatu za Njinjo, Mitole na Miguruwe hivyo yenyewe ipo makao makuu ya tarafa. Shule ipo karibu kabisa na Mbuga ya wanyama ya Selous.

2. KUANZISHWA
Shule ya sekondari Njinjo ni shule ya kata iliyoanzishwa mwaka 2007 wakati wa uanzishwaji wa shule za kata.

3. ENEO NA MAZINGIRA
Shule ina eneo lenye ukubwa wa heka 50 tambarare kabisa hivyo ina pori kubwa kabisa. Ardhi yake ni nyekundu kiasi ili tambarare sana kiasi cha kuweza kuanzisha viwanja vya michezo eneo lolote bila kusawazisha.

Mazingira ya shule ni yenye kuvutia mno yaliyopambwa kwa majengo yaliyopangiliwa kwa ustadi mkubwa, miti ya asili, miti ya vivuli iliyopangiliwa vizuri, miti ya matunda iliyotolewa na haki elimu pamoja na bustani zenye kuvutia.

Pia mazao kama mbaazi na Migomba yanafanya mazingira ya Shule yawe ya kipekee na yenye kupendeza macho.

4. IDADI YA WANAFUNZI NA WAFANYAKAZI
Shule kwa sasa ina jumla ya wanafunzi 201 ambao kati yake wasichana ni 106 na wavulana ni 95. Pia ina walimu 11 kati yao wanawake ni 4 na wanaume ni 7 na ina wafanyakazi wasio walimu(hawajaajiliwa) 2 mpishi na mlinzi.

5. HUDUMA YA AFYA, MAJI NA UMEME
Ukiwa Njinjo utapata huduma za afya kwenye kituo cha afya Njinjo kilicho km 6 kutoka shuleni pia kuna zahanati katika vijiji vya Kisimamkika na Kipindimbi. Eneo linasumbuliwa na ugonjwa mmoja tu hasa wa Malaria ambao hata hivyo ukitumia kinga unaweza kuepukika.

Shule ina mradi mkubwa wa maji uliopatikana kwa ufadhili wa Pan african unaofanya maji yapatikane wakati wote na bure kabisa kwani ni kisima kinachotumia umeme jua. Maji yamesambazwa kwa bomba shule nzima yaani kota za wafanyakazi, hosteli, Eneo la madarasa, Karibu na choo na nyingine ya wanajamii wa nje ya shule.

Shule ina umeme wa aina 2; Mosi umeme jua uliokuwa unatumika mwanzo na ulifadhiliwa na Pan African na pili ni umeme wa Tanesco. Umeme umesambazwa Nyumba za wafanyakazi, Hostelu ya wasichana na madarasani.

6. MIUNDOMBINU
Shule ya sekondari Njinjo ina vyumba 8 vya madarasa vinavyotosheleza mahitaji kutokana na idadi ya wanafunzi, ina vyoo vyilivyojengwa kwa zege vya wasichana na wavulana, hosteli ya wasichana na Nyumba nne za wafanyakazi. Maabara zimeanza kujengwa.

7. CHAKULA
Shule inatoa bure huduma ya chai kwa wanafunzi wote na ipo kwenye mpango kuanzisha chakula cha mchana kwa kushirikiana na wazazi wa wanafunzi ili kuboresha taaluma katika shule


8. MAENDELEO YA TAALUMA

Shule ina michepuo mitatu ya sanaa, sayansi na biashara ikifundisha masomo 12, ndio shule pekee wilayani Kilwa yenye michepuo na masomo mengi. Shule imekuwa na ufaulu usiridhisha sana japo si duni kwani imekuwa ikipeleka wanafunzi kidato cha tano tangu mwaka 2013 hadi 2017 tulipoikia kilele kwa kupeleka wanafunzi 4 kidato cha tano kinyume na miaka ya nyuma. Changamoto kubwa inayodhorotesha taaluma katika eneo letu ni mwamko mdogo wa elimu, umbali wa makazi na shule na utoro wa wanafunzi. Pia uchache wa walimu miaka ya nyuma ulichangia pia, hata hivyo sasa uhaba wa walimu umepungua sana.

9. SERIKALI YA WANAFUNZI NA USHIRIKI WA WANAFUNZI
Katika shule ya sekondari Njinjo serikali ya wanafunzi huchaguliwa na wanafunzi wenyewe mwezi wa Julai/Agosti kila mwaka ili washiriki kwa vitendo kwenye demokrasia. Pia wanafunzi hushiriki katika uendeshaji wa shule si tu kupitia serikali yao bali pia kwa mabaraza ya shule yanayofanyika kila mwaka ili kusikiliza kero na maoni ya wanafunzi.


Moto wetu ni "Education for Bright future" yaani Elimu kwa baadaye angavu

Leo inatosha kufikia hapa maana habari za Njinjo ni ndefu na zenye kusisimua sana

Niahirishe kwa kusema
"Tukishirikiana, Mwalimu, Mzazi na mwanafunzi... Kufaulu lazima"

Njinjo inang'aa, Njoo ujionee

Ni mimi
Peter Kajolo Kapagi
Mkuu wa Mawasiliano na Teknolojia
Shule ya Sekondari Njinjo
Julai. 2017
Njinjo. Kilwa. Lindi. Tanzania

No comments:

Post a Comment